Wednesday, January 16, 2013

Wasonjo v/s Wamasai wauana tena Ngorongoro

MGOGORO wa ardhi uliodumu kwa miaka kadhaa bila kupatiwa ufumbuzi wa kudumu na serikali katika Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha umelipuka tena baina ya jamii ya Wasonjo na wafugaji wa Kimaasai na kusababisha vifo.

Mapigano hayo yametokea ikiwa ni miezi michache tangu yale ya Agosti 24 na Septemba mosi mwaka jana, katika Kijiji cha Kisangiro, eneo la Naan na kusababisha vifo vya watu saba na wengine kadhaa kujeruhiwa huku mifugo zaidi 800 ikipotea.

Akithibitisha kutokea kwa mapigano hayo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Elias Wawa Lali, alisema kuwa vurugu hizo zilianza tangu Januari 11 na kudumu hadi 13 katika Kijiji cha Yasimdito, Kata ya Samunge na kusababisha kifo cha mtu moja.
Wawa Lali alifafanua kuwa mapigano hayo yalitokea eneo la Kibala, ambapo vijana wa Kimaasai waliwavamia wale wa Kisonjo na kuanza kuwashambulia, hivyo kuibua uhasama mkubwa uliosababisha vurugu kusambaa.

“Eneo linalogombewa limekuwa likitumiwa na jamii zote mbili wakati wote ila kuna shamba lisilozidi ekari tatu mzee wa Kimaasai Kiambati Namunguku alimuuzia mzee wa Kisonjo Samuel Lurai. Sasa Lurai alituma vijana wake waende kulisafisha shamba lake hilo lakini walipofika wakakuta vijana wa Kimaasai wanaendelea na kilimo. Hapo ndipo mzozo ulianzia baada ya makundi haya kushindwa kuelewana,” alisema Wawa Lali.

Aliongeza kuwa kutokana na vurugu hizo ilibidi Lurai amfuate Namunguka ili kupata ufafanuzi ni kwanini shamba alilomuuzia linatumiwa na watu wengine, lakini wakati huo mazungumzo hayakufanyika kwani vijana (morani) wa Kimaasai walikwisha kusanyana na kuwashambulia Wasonjo.

Mkuu huyo alisema kuwa vijana wa Kisonjo nao walijibu mashambulizi, hivyo risasi zikafyatuliwa kutoka pande zote siku iliyofuata, Jumamosi hadi Jumapili polisi walipoingilia kati.

“Polisi katika mahojiano ya hapa na pale kijijini hapo walilazimika kumshikilia mwenyekiti ambaye ilidaiwa kuwa alichochea vurugu hizo pamoja na vijana wengine wawili waliobainika kuwa walitoka vijiji vya Oldonyosambu na Maaloni,” alisema.

Alisema kuwa hadi jana, kijana mmoja wa Kisonjo, Hamagwa Raphael (22) ndiye alikuwa amethibitishwa kupoteza maisha kwa kupigwa risasi sehemu ya shingo upande wa kushoto.

Wakati mkuu wa wilaya akisema hivyo, baadhi ya wananchi walisema kuwa waliokufa ni wawili na wengine kadhaa walijeruhiwa.

Wawa Lali alisema kuwa pamoja na serikali ya wilaya kufanya jitihada za kila aina ili kumaliza mgogoro huo, bado sheria ya ardhi ya sasa inawanyima nguvu ya kutumia njia mbadala kumaliza mgogoro huo na badala yake wanamngojea waziri mwenye dhamana ndiye afanye hivyo.

Kwa muda mrefu jamii hizi mbili zimekuwa kwenye mgogoro mkubwa wa ardhi kiasi cha kusababisha vurugu zilizopoteza maisha ya watu, kujeruhi na mifugo kadhaa kupotea.

---
via Jamii blog

No comments:

Post a Comment