ZURICH, Uswisi
SHIRIKISHO
la Kimaifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limeahirisha uchaguzi wa Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na mkanganyiko uliojitokeza
katika mchakato wa uchaguzi huo.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema FIFA imetuma barua ikiagiza mchakato wa uchaguzi usimame baada ya kupata malalamiko.
Amesema kutokana na mkanganyiko huo, FIFA katika barua yake ya leo (Februari 19 mwaka huu- imeambatanishwa)
imeagiza mkutano wa uchaguzi wa TFF ambao awali ulipangwa kufanyika
Februari 24 mwaka huu uahirishwe hadi hapo itakapotuma ujumbe wake
nchini.
Ujumbe huo wa
FIFA unatarajiwa kufika nchini katikati ya mwezi ujao (Machi) ambapo
utafanya tathimini ya hali hivyo, kutuma ripoti yake katika shirikisho
hilo na baadaye kutoa mwongozo wa nini kifanyike.
Rais Tenga
amewaomba radhi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kwa usumbufu uliojitokeza
kutokana na uamuzi huo wa FIFA, hivyo kwa sasa hakutakuwa tena na
mkutano huo mpaka hapo watakapopewa taarifa nyingi.
Amesema TFF
inakaribisha kwa mikono miwili uamuzi huo wa FIFA kwa sababu ni chombo
ambacho cha juu kimpira duniani, na hatua hiyo ina lengo la kuhakikisha
kuwa kila mhusika katika mchakato huo wa uchaguzi anapata haki yake.
“Nia yetu ni
kuona watu wanatendewa haki, na nia ya FIFA ni kutafuta ukweli. Hivyo
wahusika (waathirika) wajiandae, watumie wakati huu kuandaa hoja zao ili
FIFA wakifika wawasikilize, wapate maelezo ya kina kuhusu utaratibu na
malalamiko yaliyotolewa,” alisema Tenga.
Rais Tenga
amesema timu hiyo ya FIFA itakapofika yenyewe ndiyo itakayopanga
izungumze na nani kwa wakati gani, hivyo ni vizuri waathirika na vyombo
vyote vilivyohusika na mchakato wa uchaguzi wakajiandaa.
Amesema
ilikuwa ni muhimu suala hili likatatuliwa katika ngazi ya FIFA kwa lengo
la kuhakikisha uchaguzi utakapofanyika TFF inaendelea kuwa chombo
kimoja badala ya kurudi katika migogoro iliyokuwepo huko nyuma.
“Nataka
tubakie kama tulivyokuwa. Malumbano yaishe. Pangeni hoja, wakija hao
waheshimiwa (FIFA) muwaambie. FIFA ni chombo cha juu, nafurahi
wamekubali kuingia katika hili, kwani wana shughuli nyingi wangeweza
kukataa,” amesema.
Kuhusu fursa
ya kufanya marejeo (review) kwenye Kamati ya Rufani ya Uchaguzi
inayoongozwa na Idd Mtiginjola ambayo aliielezea Jumamosi, Rais Tenga
amesema kwa vile hicho ndicho chombo cha mwisho nchini katika masuala ya
uchaguzi alishauriwa kuwa kingeweza kufanya review.
“Kwa vile
hakuna chombo kingine, nikashauriwa kuwa kinaweza kufanya review. Katika
utaratibu wa kutoa haki, uamuzi ni lazima uwe wa wazi kwa kutoa sababu.
Nilidhani hilo linawezekana, kwani Mahakama Kuu hufanya hivyo. Kwa hili
uamuzi wa Mtiginjola ni sahihi,” amesema Rais Tenga.
Kamati ya
Mtiginjola iliyokutana jana (Februari 18 mwaka huu) ilitupa maombi ya
review yaliyowasilishwa mbele yake na waombaji uongozi watano kwa vile
hakuna kipengele chochote kwenye Katiba ya TFF na Kanuni za Uchaguzi
kinachotoa fursa hiyo.
Waombaji hao
walikuwa Jamal Emil Malinzi aliyeenguliwa kugombea urais wa TFF na Hamad
Yahya aliyeondolewa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania uenyekiti wa Bodi
ya Ligi Kuu (TPL Board).
Wengine ni
walioomba kuwania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF na Kanda zao
kwenye mabano; Eliud Peter Mvella (Iringa na Mbeya), Farid Salim Nahdi
(Morogoro na Pwani) na Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu).
No comments:
Post a Comment