Monday, February 25, 2013

SERIKALI YAFUTAUSHAHIDI KWENYE KESI DHIDI YA SH.PONDA

Imeandikwa na Happiness Katabazi

HATIMAYE upande wa Jamhuri katika kesi ya uchochezi na kuiba malighafi zenye thamani ya Sh. milioni 59 inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake 48, umetangaza rasmi kuifunga kesi yake.

Hayo yalisemwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka mbele ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, muda mfupi baada ya shahidi wa 17 wa upande wa Jamhuru D/C F8586 Ismail wa kituo cha Polisi Chang’ombe kumaliza kutoa ushahidi wake ambapo  jumla ya mashahidi watatu kwa mpigo walitoa ushahidi wao.

Wakili Kweka alieleza kuwa hadi kufikia juzi upande wa  Jamhuri ulikuwa umeleta mashahidi 17 na vielelezo 13 ambavyo vilipokelewa mahakamani kama vielelezo vimetosheleza upande wa Jamhuri kufikia uamuzi huo wa kuifunga kesi yao.

Baada ya wakili Kweka kutoa maelezo hayo wakili wa Ponda, Juma Nassor aliiomba mahakama iwapatie muda hadi Machi 4 ili waweze kwenda kujiandaa na kufanya utafiti utakaowawezesha kuwasilisha maombi ya kuwaona wateja wao wote 49 hawana kesi ya kujibu.

Hata hivyo, Hakimu Nongwa alisema jukumu la kupanga tarehe ya kuja kufanya majumuisho ya mawakili wa pande hizo mbili katika kesi hiyo ya kuwaona washitakiwa wanakesi ya kujibu au la ni vyema ikaachiwa mahakama. Hakimu huyo akatoa amri kuwa majumuisho hayo yatafanyika Februali 27, 2013, saa mbili asubuhi  na kuutaka upande wa utetezi  kuwa wa kwanza kuwasilisha majumuisho yao kwa njia ya mdomo.

Kabla ya Hakimu Nongwa kukubali ombi la upande wa Jamhuri majira ya saa nane mchana, la kuifunga kesi yake, alisikiliza ushahidi wa mashahidi watatu wa waliokuwa wameletwa na upande wa Jamhuri ambao ni shahidi wa 15 ambaye ni F3929 D/C  Constebo Eliaeli (35), shahidi wa 16 ambaye ni Stationi Sajenti  Amos wa kituo cha Polisi Kati na Shahidi wa 17 ambaye ni askari mpelelezi Na. F8586 D/C Ismail.

Kwa upande wake shahidi wa 17, D/C Ismail aeleza mahakama kuwa Oktoba 17 mwaka jana, alipewa kazi na Mkuu wake wa kazi  na saa 2-9 alasiri alikuwa katika kituo cha Polisi Kijinyoma alipewa jukumu la kuwahoji washitakiwa ambao walikamatwa katika kiwanja cha Chang’ombe Marskas  wakikabiliwa na makosa ya kuingia kwa jinai katika kiwanja hicho .

Ismail alidai kuwa yeye alimhoji mshitakiwa aitwaye  Fiswaa ambaye alimweleza kuwa kati ya tarehe, mwezi na saa isiyofahamika akiwa nyumbani kwake Mlandazi Mkoani Pwani, akiwa anasikiliza Redio Iman, alisikia tangazo lilokuwa likiwataka waumini wa dini ya Kiislamu kwenda kuongeza nguvu ya kujenga msikiti katika kiwanja cha Chang’ombe Markas ambacho ni mali ya waislamu na si BAKWATA, lakini kilikuwa kimevamiwa.

Shahidi huyo alidai kuwa, mshitakiwa huyo alimweleza kuwa  aliitikia wito huo na kufunga safari toka nyumbani kwake Mlandizi na kwenda hadi kwenye kiwanja hicho kilichopo Dar es Salaam, na kuungana na wenzake ambapo kiongozi wao aliyekuwa akiwaongoza walipokuwa kwenye kiwanja hicho ni mshitakiwa wa kwanza ambaye ni  Sheikh Ponda.

“Sululu, mapanga vilitumika kama vifaa vya kujengea msikiti wa muda  katika kiwanja hicho  na ndipo usiku wa kuamkia Oktoba 17 mwaka jana, tukiwa tumekaa kwenye kiwanja hicho nikasikia sauti ikisema kuwa panda kwenye gari, panda kwenye gari na sikuwa na kumbukumbuku yoyote...,’ alidai Ismail kuelezwa na Fiswaa. Maelezo ya mshitakiwa huyo yalipokelewa kama kilelezo cha 13 na hakikupingwa na mawakili wa utetezi.

Kwa upande wake shahidi wake Shahidi wa 16, Station Sajenti Amos, alidai kuwa Oktoba 17 mwaka jana alipewa jukumu la kumhoji mshitakiwa Hussein Ally  ambaye mshitakiwa huyo alimweleza kuwa alipokea maelekezo kutoka kwa Masheikh wake wa Msikiti wa Kinyerezi yakimtaka afike katika kiwanja cha Markas na alienda akakutana na wenzake ambapo walianza kufanya usafi  ili waweze kujenga msikiti na walikuwa wakiongozwa na Sheikh Ponda kufanya ujenzi na usafi katika kiwanja hicho ambacho tayari mashahidi wengine kutoka BAKWATA walishasema kiwanja hicho ni mali ya kampuni ya Agritanza Ltd, na siyo BAKWATA tena. Maelezo ya mshitakiwa hayo yalipokelewa kama kielelezo cha 12.

Aidha, shahidi wa 15 , D/C Constebo Elieli  alidai kuwa Oktoba 17 mwaka jana, alipewa jukumu na mkubwa wake wa kazi la kuandika maelezo ya mshitakiwa Mohamed Ramadhan ambaye alimweleza kuwa siku hiyo yeye alikwenda kusali katika eneo la kiwanja hicho akitoa Oysterbay Dar es Salaam. Elieli alieleza kuwa mshitakiwa huyo alimweleza kuwa alifikia uamuzi wa kwenda kusali swala ya alfajiri hapo Chang’ombe Markas kwa sababu alikuwa anauguliwa na ndugu yake anayeishi Keko. Yeye mshitakiwa hakutaka kwenda kuswali Msikiti ya Keko kwa sababu hali ya usalama ilikuwa mbaya na hivyo akaamua kwenda kusali katika eneo hilo la Markas.

“Mshitakiwa huyo akanieleza eti baada ya kusali hapo alfajiri ya Oktoba 17 mwaka jana, ndiyo ghafla alishitukia anakamatwa na mapolisi. Nilipomhoji kama analifahamu vuguvugu la Waislamu kudai haki zao, mshitakiwa huyo alikubali kulifahamu vuguvugu hilo na kwamba yeye pale kwenye lile eneo alipokamatiwa alikuwa katika kutetea  na kudai haki yao ya kurejeshewa kiwanja kile ambacho ni mali ya Waislamu na si BAKWATA,” alidai Elieli. Hata hivyo, mahakama ilikataa kuyapokea maelezo hayo kama kielelezo kwa sababu yana dosari nyingi za kisheria.

Awali Oktoba 18 mwaka jana, ilidaiwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo na wakili Kweka mbele ya Hakimu Nongwa kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa matano likiwemo kosa la kula njama,wizi wa malighafi zenye thamani ya Sh. milioni 59 na uchochezi ambalo linamkabili Ponda na mshitakiwa wa tano, Sheikh Mkadam Swalehe ambao wanaendelea kuzuiliwa gerezani kwa sababu Mkurugenzi wa Mashitaka, DPP, Dk Eliezer Feleshi bado hawajaondolea hati ya kuwafungia dhamana.


via:wavuti.com

No comments:

Post a Comment