Tanzania imeingia makubaliano na
Kampuni ya Ujenzi(Merchants Holding Company), kutoka China kwa ajili ya
ujenzi wa Bandari Mpya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Akizungumza na wandishi wa
habari jijini Dar es Salaam jana, WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
Uwekezaji na Uwezeshaji, Mary Nagu, alisema makubaliano ya awali
yalifanyika Septemba 5 mwaka huu.
Alisema ujenzi
huo unaenda sambamba na uendelezaji wa miradi mingine inayoambatana na
ujenzi wa bandari hiyo kwenye Eneo Maalumu la kiuchumi la Bagamoyo
(SEZ),
“Leo tunashuhudia uzinduzi rasmi
wa kikosi kazi cha pamoja kati ya serikali ya Tanzania na Kampuni ya
China Merchants Holding Company kitakachosimamia utekelezaji wa mradi
huu”alisema Dk Nagu.
Dk Nagu alisema kikosi kazi
hicho kilichozinduliwa kitasimamia miradi itakayojumuisha ujenzi wa
barabara itakayounganisha bandari hiyo, mtandao wa barabara nyingine
pamoja na ujenzi wa Reli itakayounganisha bandari hiyo na Reli ya kati
na TAZARA.
Alibainisha kuwa miradi hiyo
itatekelezwa kwenye maeneo hayo maalu ya kiuchumi(Bagamoyo SEZ), hivyo
huo ni mradi wenye umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya Taifa ikizingatiwa
kwamba bandari hiyo mpya itasaidia kupunguza msongamano wa mizigo kwenye
Bandari ya Dar es Salaam ambayo tayari imekaribia ukomo wake wa
kupanuliwa.
Akifafanua zaidi, Dk Nagu
alisema jukumu hilo, linatokana na kulingana kwa Kaulimbiu ya Mkutano wa
Tano wa Mawaziri wa Nchi 50 za Kiafrika.
“Jukwa hilo linaitwa ushirikiano wan chi za Afrika na China (FOCAC), ambalo ndiyo chimbuko la mradi huu”alisema Dk Nagu.
Aliongeza kuwa mradi mpya
utakuza kwa kiasi kikubwa ushindani wa Tanzania Kikanda na Kimataifa kwa
kuzingatia kwamba itaongeza uwezo wa kuhudumia shehena za mizigo kutoka
na kwenda nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, Congo (DRC),
na Malawi.
Pia itaongeza mapato yatokanayo
na biashara ya kimataifa na kuongeza fursa za ajira hivyo kuchangia kwa
kiasi kikubwa kuongeza kasi ya kukua kwa uchumi wa nchi.
No comments:
Post a Comment