Sunday, March 3, 2013

SIMBA NA LIBOLO MAMBO YAMEIVA


 


·       Liewig aahidi kupambana hadi mwisho

·       Poppe aahidi mamilioni kwa wachezaji

·       Kapombe asema Sunzu atawaua Waangola

Na Ezekiel Kamwaga, Kwanza Sul, Angola

KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Jean Elysee Liewig, amesema ana matumaini timu yake itapata matokeo mazuri katika mchezo wa kesho baina ya Wekundu wa Msimbazi na Libolo ya Angola.

Mechi hiyo imepangwa kuchezwa kesho kuanzia saa tisa alasiri katika Uwanja wa Estadio Libolo, uliopo katika mji mdogo wa Calulo jimbo la Kwanza Sul.

Katika mechi ya kwanza baina ya timu hizo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita, Simba ilifungwa 1-0 na mabingwa hao wa Angola.

Hata hivyo, Liewig alisema ingawa matokeo ya kufungwa nyumbani hayakuwa mazuri, ana imani Simba nayo inaweza kufanya vizuri ugenini.

“Kama wao walitufunga kwetu kwanini sisi tusiwafunge kwao. Ukiangalia kwenye ile mechi ya kwanza wao walipata nafsi moja tu ya maana na wakaitumia. Sisi tulipata nafasi kama tatu hivi na hatukutumia vizuri hata moja,” alisema.

Liewig alisema ameridhishwa na ari na mazoezi mazuri ambayo Simba imefanya kwa wiki nzima kujiandaa na mechi hiyo na kwamba kuna dalili kuwa timu yake inaweza kufanya lisilotarajiwa.

Akizungumza na wachezaji katika kikao kilichofanyika katika Hoteli ya Anisaan Ritz ambako Simba imefikia, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Zacharia Hans Poppe, alitoa ahadi ya Sh milioni 10 iwapo watafanikiwa kuitoa Libolo.

Aliwataka wachezaji wa Simba kuwakumbuka mamilioni ya washabiki wao waliopo Tanzania ambão hawalali wala kula vizuri wakati timu yao kipenzi inapokuwa na matokeo mabaya.

Poppe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba na pia kundi la Friends of Simba, alisema ana imani kubwa na wachezaji wa timu yake kwa vile ndiyo bora Tanzania na kama wataamua kucheza kwa nguvu zao zote, matokeo mazuri yanawezekana.

“Nyie ni wachezaji wazuri sana. Kama nyote mtacheza kama timu na mkacheza kwa uwezo wenu wote, ni wazi kwamba mnaweza kuibuka na ushindi,” alisema.

Akizungumzia mechi ya kesho, nahodha msaidizi wa Simba, Shomari Kapombe, alisema mechi baina yao na Libolo itakuwa tofauti na ya kwanza kwa sababu ya kuwepo kwa mshambuliaji Mzambia, Felix Sunzu.

“Tulimkosa sana Sunzu kwenye mechi ya Dar es Salaam. Mipira ilikuwa haikai kule mbele na hilo lilikuwa tatizo kubwa, kubwa sana na hiyo ni kwa sababu Sunzu hakuwepo. Nadhani sasa tuna nafasi zaidi kuliko mara ya kwanza,” alisema.


WAKATI  HUO  HUO IMEELEZWA  KUWA MWAMUZI  ALIYECHEZESHA SIMBA NA SHANDI KUCHEZESHA NA 
Na Ezekiel Kamwaga, Angola

MWAMUZI Nhleko Simanga Pritchard kutoka nchini Swaziland ambaye alichezesha mechi baina ya Wekundu wa Msimbazi na Al Ahly Shandi ya Sudan mwaka jana, ndiye atakayechezesha mechi ya kesho dhidi ya Libolo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyopatikana kutoka Chama cha Soka cha Angola leo asubuhi, mwamuzi huyo atasaidiwa na na wenzake Mkhabela Bhekisizwe, Mbingo Petros na Fabudze Mbongiseni ambão wote wanatoka Swaziland.

Kati ya hao, ni Nhleko na Petros pekee ambão ndiyo waliochezesha mechi ya Shandi ambayo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 yaliyofungwa na Haruna Moshi (77), Patrick Mafisango ambaye sasa ni marehemu (88) na Emmanuel Okwi (90).

Wachezaji wote hao watatu waliofunga katika pambano hilo hawatacheza katika mechi ya Libolo kwa sababu tofauti. Mafisango alifariki kwa ajali siku mbili baada ya kurejea kutoka Sudan kwenye mechi ya marudiano ambako Simba ilitolewa.

Okwi amehamia katika klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia na Boban ameshindwa kusafiri na timu kwenda Angola kwa sababu ya kushikwa na malaria kali.

Kamisaa wa pambano hilo lililopangwa kuanza majira ya saa tisa kamili kwa saa za hapa (sawa na saa 11 jioni kwa saa za Tanzania) anatarajiwa kuwa Mandla Mazibuko kutoka nchini Afrika Kusini.

No comments:

Post a Comment